MAOFISA UGANI WATAKIWA KUWA NA SHAMBA LA MFANO LA ALIZETI KWA AJILI YA KUFUNDISHIA WAKULIMA
SERIKALI imewaagiza Maafisa Ugani wa Kata na Kijiji kuwa na shamba la mfano la alizeti ili kuwafundisha kwa vitendo wakulima na kuongeza uzalishaji wa zao hilo nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Kilimo, Prof Adolf Mkenda
Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma wakati akifungua mkutano wa maafisa ugani kuhusu
kanuni bora za alizeti kwa maafisa hao kutoka Mikoa ya Singida, Dodoma na
Manyara.
Prof Mkenda amesema kama nchi ina changamoto mbili ambapo
moja ni kuzalisha sana mafuta na nyingine ni kutafuta wanunuzi ili kuweza
kufanikisha kudhibiti suala zima la uhaba wa mafuta.
Kutokana na hilo amesema maafisa Ugani wanakazi kubwa ya
kuhakikisha wanatoa elimu ya uzalishaji zao la alizeti kwa vitendo kupitia
mashamba darasa ambayo wanatakiwa kuwa nayo.
"Tuna changamoto ya uzalishaji, hatuzalishi vya kutosha
ingawa uwezo wa kuzalisha tunao,hivyo kila afisa Ugani anapaswa kuwa na shamba
darasa ili afundishe wakulima kwa vitendo katika eneo analofanyia kazi ili
waweze kuzalisha kwa kiasi kikubwa,”Amesema Prof Mkenda.
Waziri Mkenda amesema lengo ni kuona Serikali inaepuka
kutumia fedha nyingi kwa ajili ya kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi badala
yake yapatikane kwa wazalishaji wa hapa nchini.
"Ni lazima tutatue kitendawili hiki kuanzia zao moja
hadi lingine ikiwemo kutoa elimu na kuwapa pembejeo wakulima ili kufanikisha
kuondokana na uzalishaji mdogo,” Amesema Prof Mkenda.
Nae Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mpwapwa, George Fuime
amebainisha kuwa haiwezekani kama nchi kulima zao la Alizeti kwa wingi lakini
upatikanaji wa mafuta unakua mdogo hivyo amewataka maafisa ugani kuhakikisha
wanatoa mafunzo hayo kwa vitendo kwa wakulima.
Fuime amesema ni vema wakatumia nafasi yao kutoa elimu ili
wakulima wajue nini wanatakiwa kufanya ili waweze kuzalisha kwa tija.
CHANZO: MICHUZI TV
Comments
Post a Comment